MAUTI YA KI-ROHO

Kufa ki-Roho


Nanyi mlikuwa wafu Kwa sababu ya makosa na dhambi zenu, ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi. Zamani sisi sote nasi tulienenda kati yao katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine (maneno mepesi kukazia). Waefeso 2:1-3



Bila shaka Paulo alikuwa hazungumzii kifo cha kimwili kwa sababu alikuwa anawaandikia watu waliokuwa hai kimwili. Lakini akasema, hapo zamani walikuwa “wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zao.” Dhambi hufungua mlango wa kifo cha kiroho (tazama Warumi 5:12). Kuwa wafu kiroho maana yake ni kuwa na asili ya dhambi rohoni mwako. Ona maneno ya Paulo kwamba, “kwa tabia” wakawa watoto wa hasira.



Tena, kufa kiroho maana yake kuwa na asili ya Shetani katika roho yako kwa namna fulani. Paulo alisema kwamba wale wote waliokufa kiroho wana roho ya “mkuu wa uwezo wa anga” ikitenda kazi ndani yao. Huyo “mkuu wa uwezo wa anga” ni Shetani (tazama Waefeso 6:12), na roho yake inatenda kazi ndani yao wote ambao hawajaokoka.



Yesu aliwaambia hivi Wayahudi waliokuwa hawajazaliwa mara ya pili:



Ninyi ni wa baba yenu Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo, wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe, kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo (Yohana 8:44).



Kwa upande wa kiroho, wale ambao hawajazaliwa tena si tu kwamba wana asili ya Shetani katika roho zao, bali Shetani ni baba yao wa kiroho pia. Basi, ni kawaida kwao kutenda kama shetani. Wao ni wauaji na waongo.



Si kwamba watu wote ambao hawajaokoka wamefanya mauaji, bali ni kwamba wanahamasishwa na chuki ile ile kama ya wauaji, nao wangeweza kuua kama wangefanikiwa. Kuhalalishwa utoaji mimba katika nchi nyingi ni uthibitisho wa kweli hiyo. Watu ambao hawajaokoka wataua hata watoto wao wenyewe, ambao bado hawajzaliwa!



Hii ndiyo sababu mtu lazima azaliwe tena kiroho. Inapotokea hivyo, hiyo asili ya dhambi na kishetani huondolewa katika roho yake, na nafasi yake huchukuliwa na asili ya Mungu takatifu. Roho Mtakatifu wa Mungu huja na kukaa ndani ya roho yake. Hawi “mfu kiroho” tena, bali anafanywa “hai kiroho”. Roho yake haiwi imekufa tena bali inakuwa hai kwa Mungu. Badala ya kuwa mtoto wa kiroho wa Shetani, anakuwa mtoto wa kiroho wa Mungu.



Matengenezo Si Kuzaliwa Upya



Kwa sababu watu ambao hawajaokoka wamekufa kiroho, hawawezi kuokolewa kwa matengenezo, hata kama watajaribu kiasi gani. Watu ambao hawajaokoka wanahitaji asili mpya, si matendo mapya ya nje tu. Unaweza kumchukua nguruwe, ukamsafisha vizuri akawa safi, ukampulizia hata manukato na kumfungia tai ya rangi nzuri tu shingoni mwake, lakini mwisho wa siku ulicho nacho ni nguruwe aliyesafishwa tu! Bado asili yake ni ile ile. Na hautapita muda mrefu kabla hajaanza kunuka vibaya tena na kulala kwenye matope tena.



Ndivyo ilivyo kwa watu washika dini sana ambao hawajawahi kuzaliwa tena. Wanaweza kuwa wasafi kwa nje, lakini ndani ni wachafu tu kama kawaida. Yesu alisema hivi kwa watu washika dini wa siku Zake:



Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe chanu, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu! Safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi! Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi: Kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi! (Mathayo 23:25-28). inaandelea mauti ya kiroho k'2

Blog Archive

Followers