MAFUNDISHO YA KUISHI MAISHA MATAKATIFU

JE ? NIMAISHA YAPI TUNAYOSTAHILI KUISHI

Ni watu  wangapi wangeona wameheshimiwa sana kama mtu angewaita “mhubiri wa utakatifu”? Ni wangapi wanaojiita Wakristo wangetumia maneno hayo kwa njia ambayo si ya kudhihaki? Mbona utakatifu ni somo baya sana mawazoni mwa watu wengi wanaodai kuamini kitabu ambacho kina maneno mtakatifu au utakatifu zaidi ya mara mia sita, chenye kuwaahidi wakati ujao katika mji mtakatifu ambamo ndani yake anakaa “Aliye mtakatifu”, ambaye jina Lake ni mtakatifu, anayewapa Roho Wake Mtakatifu na ambaye kiti Chake cha enzi kitakatifu kimezungukwa na wenye uhai wanne wasioacha kusema usiku na mchana, “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Mungu Mwenyezi”? (ona Ufunuo 21:2; Isaya 40:25; Walawi 22:32; 1Wathes. 4:8; Zaburi 47:8; Ufunuo 4:8 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).



Kama sehemu ya kwanza ya Mahubiri ya Mlimani imetufundisha kitu, ni kwamba Yesu alikuwa mhubiri wa utakatifu. Hiyo ndiyo iliyokuwa mada Yake – utakatifu, na jinsi unavyohusiana na wokovu.



Mahubiri ya Mlimani yameandikwa katika Injili ya Mathayo sura ya 5, 6 na 7. Mpaka sasa tumetazama sura ya 5 tu. Hapo, katika zile “Heri” tulijifunza tabia au sifa za wanaokwenda mbinguni. Pia tuligundua kwamba Yesu hakuja kuibatilisha au kuiondoa Torati, na kwamba kushika sheria ni muhimu sana. Tulijifunza kwamba hatuwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni kama haki yetu haitazidi ile ya waandishi na Mafarisayo, walioishika sheria kama ilivyokuwa ila wakapuuza maana yake.



Sehemu ya pili ya Mahubiri ya Mlimani – yaani Mathayo 6 na nusu ya kwanza ya sura ya 7 – ina amri zingine tena ambazo Kristo aliwapa wafuasi Wake. Je, kuzishika kunahusika kwa lolote na wokovu? Hakika kabisa. Sehemu ya mwisho ya sura ya saba inaonyesha jambo hilo waziwazi kabisa, kama tutakavyoweza kujionea.



Hebu tuendelee kusoma yale ambayo Yesu aliwaagiza wafuasi Wake wa kweli, ambao waliamini kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu, ni Masiya. Tujiulize swali hili, zito kabisa: Ikiwa wasikilizaji wa Yesu hawakumwamini, walimtii kwa sababu gani? Mbona watake hata kusikiliza akifanya madai ambayo yangeathiri kila eneo la maisha yao? Jibu ni wazi: Kwa kuwa waliamini, walitaka kutii. Wangeonyesha imani yao kwa matendo yao.





Ona katika sehemu hii ya kwanza Yesu anahesabu kwamba wafuasi Wake watatenda haki, naye anawaonya wahakikishe kwamba makusudi yao ni kumpendeza Mungu badala ya kuwapendeza watu.




“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe ya siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Mathayo 6:1-4 – Maneno mepesi kutilia mkazo).



Yesu alitazamia kabisa kwamba wafuasi Wake wangetoa sadaka kwa maskini (kama tulivyojifunza katika sura ya 3 ya kitabu hiki). Torati iliagiza hivyo (ona Kutoka 23:11; Walawi 19:10; 23:22; 25:35; Kumbu. 15:7-11), na waandishi na Mafarisayo walifanya hivyo kwa kupiga matarumbeta, kwa kusudi la kuwafanya watu maskini waone utoaji wao. Lakini – ni wangapi wanaojiita Wakristo (na hata makanisa ya Kikristo) wanaotoa chochote kwa maskini? Hawajafikia hata mahali pa kutaka kuchunguza makusudi yao ya utoaji zaka! Kama uchoyo na ubinafsi uliwasukuma waandishi na Mafarisayo kutangaza kutoa kwao sadaka, ni nini kinachowasukuma wanaojiita Wakristo kupuuza hali ya maskini? Je, haki yetu inazidi ile ya waandishi na Mafarisayo?



Kama ambavyo Paulo atarudia katika 1Wakorintho 3:10-15, tunaweza kufanya matendo mema ambayo hayatapata thawabu ikiwa nia na makusudi yetu si safi. Wafuasi wa kweli wa Kristo wanapaswa kuwa na nia safi katika kila tendo jema, lakini si wote walio nayo. Paulo aliandika kwamba inawezekana hata kuihubiri Injili kwa makusudi yasiyo safi (ona Wafilipi 1:15-17). Njia iliyo bora ya kuhakikisha kwamba kutoa kwetu kunasukumwa na makusudi safi ni kutoa kwa siri kiasi iwezekanavyo.



Yesu pia aliwatazamia wafuasi Wake waombe na kufunga. Hiyo ilikuwa lazima. Hakusema “Kama mtaomba”. Alisema “Mwombapo”. Hatari ilikuwa wangeweza kuyaruhusu makusudi yao kuchafuka, kama ilivyokuwa kwa makusudi ya wasioamini waliokuwa wanaomba na kufunga. Kama hayo yangetokea, wangepoteza thawabu ile ambayo wangepata kama makusudi yao yangekuwa safi. Basi aliwapa mashauri yafuatayo:



“Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayoyahitaji kabla ninyi hamjamwomba…”



“Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso, ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Mathayo 6:5-8; 16-18).



Narudia tena: Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo ambao hawatumii muda wao mwingi katika maombi, na ambao hawajawahi kufunga kabisa? Haki yao inalinganishwaje na haki ya waandishi na Mafarisayo, ambao walifunga na kuomba (japo kwa sababu mbaya)?



Maombi aliyoagiza yesu tuyafanye :

Yesu pia aliwaambia wanafunzi Wake jinsi walivyotakiwa kuomba. Maombi Yake mfano ni ufunuo wa hali ya juu sana kuhusu matazamio Yake kwa habari ya pendo lao, utii wao na vipaumbele.



“Basi ninyi salini hivi: ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu’.” (Mathayo 6:9-11)



Jambo la kwanza muhimu sana kwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu iwe jina la Mungu litukuzwe. Yaani, jina la Mungu liheshimiwe, liabudiwe na kutakatifuzwa.



Bila shaka wale wanaoomba kwamba jina la Mungu litukuzwe wanatakiwa wao wenyewe kuwa watakatifu, wanaolitukuza jina la Mungu. Itakuwa ni unafiki kufanya vinginevyo. Kwa hiyo, sala hii inaonyesha shauku yetu kwamba na wengine wajinyenyekeze kwa Mungu kama ambavyo sisi tumefanya. Na – kama nilivyouliza katika sura nyingine hapo nyuma – mtu anaonyeshaje kiwango cha shauku yake kwamba anataka jina la Mungu litakaswe kama anajistarehesha kwa kutazama picha ambazo zinachezwa na wachezaji wenye kutumia vibaya jina la Mungu na la Mwana Wake? Kulingana na uchunguzi wangu, hiki ni kitu ambacho wengi wanaojiita Wakristo hufanya mara kwa mara. Je, wewe ungechukizwa na sinema ambayo waigizaji wanatumia jina lako kama neno la kuapa au kushangaa?



Ombi la pili katika sala hiyo linafanana na la kwanza: “Ufalme wako uje.” Wazo la ufalme huonyesha kwamba kuna Mfalme anayetawala ufalme Wake. Mwanafunzi Mkristo anatamani kuona mfalme Wake – yule atawalaye maishani mwake – akitawala dunia nzima. Laiti kila mtu angepiga goti lake kwa Mfalme Yesu, katika imani tiifu!



Ombi la tatu linarudia yale mawili ya kwanza: “Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.” Hapa tena – tunawezaje kuomba kwa dhati ombi la namna hii bila sisi wenyewe kuwa tumejinyenyekeza chini ya mapenzi ya Mungu katika maisha yetu? Mwanafunzi wa kweli anatamani kwamba mapenzi ya Mungu yatafanyika duniani kama huko mbinguni – kikamilifu na kabisa.



Kwamba jina la Mungu litakaswe, na mapenzi Yake yafanyike, na ufalme Wake uje vinatakiwa kuwa muhimu zaidi kwetu kuliko chakula cha kutuhifadhi, au “riziki yetu”. Hili ombi la nne linawekwa hapo kwa sababu. Inaonyesha mpangilio mzuri wa mambo ya muhimu maishani mwetu, na hakuna dalili za uchoyo hapo. Huyu mwanafunzi anayeomba anamtumikia Mungu, si mali.

Followers