Hujapoteza kitu!
Umefanya uamuzi wa busara kuokoka kwa sababu ndani ya Yesu Kristo hakuna hasara. Wewe uwe mtendaji wa neno lake, na ndipo utakapojua na kuthibitisha ya kuwa kweli kwa Yesu Kristo kuna kila kitu unachokihitaji sasa na cha maisha ya siku zote.
Inawezekana umewahi kusikia watu wakisema mtu anapookoka anafilisika – na inawezekana umewahi kuona watu wengine waliookoka wakiwa na maisha duni. Nataka nikueleze ya kwamba haimo katika mpango wa Mungu kuwafilisi watu wake wanapookoka. Wengi wanakuwa na maisha duni kwa sababu ya kukosa mafundisho sahihi ya neno la Mungu baada ya kuokoka! Wanaangamia kwa kukosa maarifa ya neno la Mungu.
Ukichukua biblia yako na kusoma kitabu cha 2Wakorintho 8:9 utaona wazi wazi ya kuwa kati ya mambo aliyoyafanya Yesu msalabani alipokufa kwa ajili yetu – ni kuuchukua umaskini wetu ili tupate kupokea utajiri wake.
Ndiyo sababu Yesu Kristo aliwahi kuwaambia wanafunzi wake (ambao ni pamoja na wewe sasa kwa kuwa umeokoka) ya kwamba:
“ Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:29,30).
Haya ni maneno ya Yesu Kristo mwenyewe, na Roho Mtakatifu anakuletea maneno haya ndani ya moyo wako kukuondoa wasiwasi. Umeamua kuokoka – umeamua kupokea baraka kuanzia sasa.
Nataka nizidi kukutia moyo ya kuwa umefanya uamuzi wa busara kwa kuokoka. Maana umechagua baraka umeikataa laana; umechagua Uzima, umeikataa mauti; Umechagua Nuru, Umeikataa giza; Umemchagua Yesu, umemkataa shetani;Umechagua kwenda mbinguni, umekataa kwenda jehanamu!
Hata kufahamu ya kuwa ulipookoka umefanya uamuzi wa busara – ni baraka ya pekee pia! Au wewe unasemaje? – ni kweli au uongo? JIBU ni kweli maana umeamuwa wewe mwenyewe hukuamuliwa,
Kumbuka unapookoka unampokea Yesu Kristo moyoni mwako ambaye ndiye KWELI kwa hiyo nakushauri kataa uongo unaotaka kukurudisha nyuma kiroho. Umeamua kuokoka – umeamua kwa busara na uwe ni uamuzi wa kudumu!
Ndugu Mtazamaji/ MSOMAJI; Bila shaka unampenda Mungu Sana tunaamini hivyo Kwa vile ulivyoweza kufika mahali hapa tulipo kupitia Mtandao huu, lipo kusudi la Mungu kutaka kukusaidia jambo Fulani ikiwa uko tayari katika yote jiepushe na mafundisho yasiyokuwa ya ki-Mungu Mathayo 16:6-12) piga simu kwa masaada zaidi huduma hii ni bure 0757328311